SAYANSI YA “KUBALANS” SHOBO.
Shuleni hasa wakati wa elimu ya upili a.k.a sekondari ni watu wachache sana walikua wakichukua masomo ya Sayansi. Kwenye idadi hiyo ya wanasayansi kulikua na wale ambao walikua na uelewa wa nini wanachotafuta, ni kitu gani Sayansi itawasaidia, kuna waliokua na raha ya kusoma masomo mengi wakijua kwamba huenda ikawasaidia kupata daraja zuri katika matokeo ya mwisho.
Ukweli ni kwamba Sayansi ni ngumu kwa watu wengi, vitu vingi vinavyohusishwa na Sayansi pia huwa na kawaida ya kutokueleweka kwa wengi.
Kubalans shobo ni tawi la Sayansi linalohusiana na uwezo wa mtu au kikundi cha watu kutokua na mihemko kupitiliza pamoja na kutojipendekeza. Kubalans shobo ni somo gumu sana hasa katika dunia ya Sayansi na teknolojia ambako kwa kiasi kikubwa maisha ya karibia kila mtu yanaonekana ni mazuri sana kwenye mitandao. Pia, ugumu wa kubalans shobo unakuja kwenye uhitaji uliopitiliza wa kukubalika, kuonekana unajua na tamaa ya ndani ya kupata kila kizuri kwa njia za mkato; bila kuvuja jasho.
Kwa upande mwingine, wenye madaraka, umaarufu na pesa hufanya somo la kubalans shobo kutopenya kwenye vichwa vya wengi. Kwa kiasi kikubwa, watu hawa wanapenda kunyenyekewa na hurundika watu wengi karibu yao, watu ambao kwa kiasi kikubwa kazi zao ni kuwafurahisha, kuwaambia yale ambayo wanataka kuyasikia kuburudisha nafsi zao.
Ili uweze kufaulu somo la kubalans shobo, fanya yafuatayo.
1. RIDHIKA NA ISHI MAISHA YA UWEZO WAKO.
Sehemu ya kwanza kabisa kuanza ni kuridhika na hatua uliyofikia kimaisha. Ukiridhika na kile ulichonacho huku ukitafuta vingine ni dahiri kuwa hutahitaji kujilamba kwa mwenye nacho ili upate vya mteremko. Ni muhimu kugundua kuwa vitu ulivyo na uwezo navyo kwa sasa ndivyo unavyotakiwa kuwa navyo, usitake kuingia katika mfumo wa maisha ambao hauuwezi.
2. TAFUTA CHAKO.
Kama zoezi la kubalans shobo ni gumu kwako kwa sababu umezungukwa na watu wanaokusaidia kwa namna moja ama nyingine hivyo kuhitaji shobo zako ili uendelee kusaidiwa, tafuta njia ya kupata vitu vyako ambavyo vitakufanya uwe huru. Kuna uhuru na furaha ambaya huja kwa kutafuna jasho lako, usijinyime furaha hii.
3. JUA THAMANI YAKO.
Hii ni mahsusi kwa shobo zinazoelekezwa kwa jinsia ya pili. Kwa kawaida, shobo huwakwaza hata wale ambao unajitahidi sana kuwaonesha ni kwa namna gani wana umuhimu; muda mwingine unaonesha wana umuhimu mkubwa kuliko hata wewe mwenyewe. Shobo kwa kiasi kikubwa ni madhara ya kutojua thamani yako na kuweka thamani ya juu sana kwa mtu mwingine. Fanyia kazi kujua thamani yako na hutafeli somo la kubalans shobo.
4. FAHAMU MADHARA YA KUTOBALANS SHOBO.
Shobo hulemaza pande zote mbili, mtoa na mpokea shobo. Mpokea shobo kwa kiasi kikubwa anaweza kujihisi ni muhimu kuliko hali halisi. Mara zote unapokua umezungukwa na watu ambao kazi yao pekee ni kukusifia, ni dhahiri kuwa hautafahamu mapungufu yako na utaijenga akili yako katika kile ambacho wanakusifu; kwa kiasi kikubwa kuna mengi ambayo wanaongeza kukufurahisha. Mtoa shobo ataendelea kupewa nafasi kubwa kwenye maisha ya mpokea shobo licha ya ukweli kuwa hakuna anachojifunza na maisha yake kwa kiasi kikubwa yanabaki pale pale.
Jiulize ukishoboka kwa ambaye sio mpenda shobo?? Aibu itakayokukuta utaijua mwenyewe, jifunze kubalans shobo.